Home > Author > Enock Maregesi
141 " Nusu dakika baada ya kuondoa gari, Murphy aliona kiwiliwili cha mtu kikimwendea mbio kutokea katika nyumba ya magaidi! Hapohapo alisimamisha gari na kuacha taa zikiwaka, halafu akashika bunduki na kushuka – akiwa ameangalia mbele kwa tahadhari kubwa. Alikuwa mwanamke. Debbie! Murphy alipojua ni Debbie, alitupa bunduki na kuchomoka mbio mpaka wakakutana na kukumbatiana kwa nguvu! Murphy alimbeba Debbie na kumbusu kila sehemu, halafu akamfuta machozi na kumbembeleza. "
― Enock Maregesi , Kolonia Santita
142 " Ngumi ya Ambilikile ilitua barabara katika kichwa cha Brookshield na kuleta madhara makubwa. Sehemu moja ya kichwa, cha Brookshield, ilibonyea kabisa! Kimya kilichotawala kiliwasisimua mashabiki. Walipovamia ulingo, kushuhudia kisichoweza kufikirika, walitoka pale wakiwa na hakika ya asilimia 100; kwamba John alikuwa na nyundo (au chuma chochote) katika mfuko wake wa bukta – aliyoitoa (harakaharaka), wakidhani ni mtindo wa kipigo, na kumpondea mwenzake kichwani! Ile haikuwa nyundo. Wala haukuwa uchawi. Ilikuwa ngumi, imara, ya uzito wa kilo 90; uzito wote wa John Ambilikile. "
143 " Ndani ya chumba, akiwa bado amechanganyikiwa, akiwa hajui Debbie alikokwenda, Murphy alisikia walinzi wakipiga kelele nje. Kamanda huwa anakuwa shetani nyakati kama hizo. Alibeba pumzi. Mikononi mwake akiwa na M-16, Debbie kichwani; Murphy alishangaza umati wa watu! Risasi zaidi ya sitini zilifyatuka katika bunduki, mlango wote ukabomoka – ndani ya sekunde kumi! "
144 " Murphy hakupenda kupoteza muda. Alinyanyuka na kumimina risasi, Mungu akamsaidia akadondosha wawili huku wengine wakipotea kwa kuruka vibaya na kukwepa. Kwa kasi Murphy alikimbia huku ameinama mpaka katika milango mikubwa ya nje, ambayo sasa ilikuwa wazi. Hapo akasita. Chochote kingeweza kumpata kwa nje kama hangekuwa mwangalifu. Bunduki yake ilishakwisha risasi. Aliitupa na kuchungulia nje akaona adui mmoja akikatisha kwenda nyuma ambako ndiko mashambulizi yalikokuwa yakisikika sasa. Murphy hakumtaka huyo. Aligeukia ndani kuona kama kulikuwa na bunduki aichukue lakini hata kisu hakikuwepo. Akiwa bado anashangaa, ghafla alitokea adui – kwa ndani – na kurusha risasi, bahati nzuri akamkosa Murphy. Murphy, kama mbayuwayu, aliruka na kusafiri hewani hapohapo akadondoka nyuma ya tangi la gesi karibu na milango ya nje. Alipoona vile, adui alidhani Murphy alidondoka mbali. Alibung’aa asijue la kufanya. Wasiwasi ulipomzidi alishindwa kuvumilia. Alishika bunduki kwa nguvu na kupiga kelele, "Yuko hukuuu!" Halafu akajificha ili Murphy asimwone. Lakini Murphy alikuwa akimwona. "
145 " Radia Hosni alikuwa na bahati kuliko watu wote duniani. Frederik Mogens alipofika katika helikopta na kukuta Murphy na Yehuda wakihangaika kuutafuta mwili wa Radia, hakushangazwa na walichomwambia. Kwa sababu alijua nini kilitokea. Radia alikutwa akipumua kwa mbali. Hivyo, Debbie na marubani walimchukua na kumpeleka Mexico City haraka ilivyowezekana. Black Hawk waliyokuwa wakiishangaa ilikuwa ya DEA. Lakini si ile waliyokwenda nayo Oaxaca. Ilikuwa nyingine ya DEA, iliyotumwa na Randall Ortega kuwachukua Vijana wa Tume na kuwapeleka Mexico City haraka ilivyowezekana. Black Hawk waliyokwenda nayo Oaxaca ndiyo iliyomchukua Radia na Debbie na kuwapeleka Altamirano (hospitali ya tume) mjini Mexico City. Mogens angekwenda pia na akina Debbie; lakini alibaki kwa ajili ya kumlinda El Tigre, na mizigo yake, na baadhi ya makamanda wake wachache. El Tigre angeweza kutoroka kama angebaki na polisi peke yao, na Mogens hakutaka kufanya makosa. "
146 " Kama kuna swali maarufu kuliko yote katika kitabu cha 'Kolonia Santita' ni "Кто Вы, где Вы от, и почему Вы в Москве?" lililoulizwa na товарищи (Komredi) Anatoly-Chaika, baada ya kumfikisha Murphy katika 'dacha' ya Kolonia Santita ya Yugo Zapadnaya. Murphy hakumwelewa Chaika. Lakini mwenzake na Chaika (Vladimir) alipouliza kwa tafsiri, "Wewe ni nani, unatoka wapi, na unafanya nini Moscow?" Murphy alimwelewa na kucheka akiwa amenuna. Bila swali hilo asingeokoka. "
― Enock Maregesi
147 " Kiswahili ni lugha rasmi ya nchi za Tanzania, Kenya na Uganda. Ni lugha isiyo rasmi ya nchi za Rwanda, Burundi, Msumbiji na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Lugha ya Kiswahili ni mali ya nchi za Afrika ya Mashariki, si mali ya nchi za Afrika Mashariki peke yake. Pia, Kiswahili ni lugha rasmi ya Umoja wa Afrika; pamoja na Kiarabu, Kiingereza, Kifaransa, Kireno na Kihispania. Kiswahili ni lugha inayozungumzwa zaidi nchini Tanzania kuliko nchi nyingine yoyote ile, duniani. "
148 " Kiswahili ni lugha ya Kibantu na lugha kuu ya kimataifa ya biashara ya Afrika ya Mashariki ambayo; maneno yake mengi yamepokewa kutoka katika lugha za Kiarabu, Kireno, Kiingereza, Kihindi, Kijerumani na Kifaransa, kutoka kwa wakoloni waliyoitawala pwani ya Afrika ya Mashariki katika kipindi cha karne tano zilizopita.Lugha ya Kiswahili ilitokana na lugha za Kisabaki za Afrika Mashariki; ambazo nazo zilitokana na Lugha za Kibantu za Pwani ya Kaskazini Mashariki za Tanzania na Kenya, zilizotokana na lugha zaidi ya 500 za Kibantu za Afrika ya Kusini na Kati.Lugha za Kibantu zilitokana na lugha za Kibantoidi, ambazo ni lugha zenye asili ya Kibantu za kusini mwa eneo la Wabantu, zilizotokana na jamii ya lugha za Kikongo na Kibenue – tawi kubwa kuliko yote ya familia ya lugha za Kikongo na Kinijeri katika bara la Afrika. Familia ya lugha za Kikongo na Kibenue ilitokana na jamii ya lugha za Kiatlantiki na Kikongo; zilizotokana na familia ya lugha za Kikongo na Kinijeri, ambayo ni familia kubwa ya lugha kuliko zote duniani kwa maana ya lugha za kikabila.Familia ya lugha ya Kiswahili imekuwepo kwa karne nyingi. Tujifunze kuzipenda na kuzitetea lugha zetu kwa faida ya vizazi vijavyo. "
149 " Lakini Kiswahili kilizaliwa Afrika Mashariki. Kwa nini hatuithamini lugha yetu? Kwa nini hatuzithamini lugha zetu za makabila? Kwa nini hatuipendi na kuitetea lugha yetu ya taifa ambayo ndiyo lugha ya biashara na mawasiliano ya Afrika Mashariki? Kwa nini hatuvitetei vizazi vijavyo kwa kuvitetea vizazi vya leo? "
150 " Kiingereza kililetwa na wakoloni wa Kiingereza kutoka Uingereza na walikitumia katika masuala yote ya kiutawala ya Afrika Mashariki. Kililetwa pia na wamisionari waliojenga shule na kuwafundisha Kiingereza wanafunzi na walimu na watu wengine wa kawaida, kwa lengo la kuwasaidia katika kazi yao ya kueneza dini kama wakalimani, hivyo kufanya Kiingereza kienee zaidi kuliko Kiswahili. "
151 " Komandoo Nicolas Kahima Kankiriho ('Kahima the Warrior') alizaliwa katika Wilaya ya Bushenyi, Ankole, kusini-magharibi mwa Uganda, Julai 24, 1954, mtoto wa tano kuzaliwa, katika familia ya watoto sita ya Nicodemas Kankiriho; mzee wa heshima wa Wabaima, aliyekuwa akisifika sana kwa uchungaji (wa mifugo) na msisitizo mkali wa ukiristo kwa watoto wake wote; hasa Kahima na Yebare, binti yake wa pekee, aliyekuwa wa mwisho kuzaliwa.Kahima (futi 6 inchi 3 aliyekuwa akiongea Kinyankole, Kiswahili, Kiingereza na Kihispania kwa ufasaha), baada ya kutoka Uganda – kwa mafunzo ya mwanzo ya ukomandoo ya Kiisraeli – alikwenda Urusi na Korea ya Kaskazini ambako aliongeza ujuzi hadi kiwango cha juu kabisa; kabla ya kwenda Amerika ya Kusini, kama askari wa msituni wa vyama vya kisiasa visivyo rasmi vya magorila wa Kolombia.Akiwa Kolombia, Kahima alikutana na Eduardo Chapa de Christopher (kiongozi wa zamani wa Kateli ya Diablos de Amazonas, Mashetani wa Amazoni, iliyokuwa ikivilinda vyama vya kisiasa vya magorila vya Americas) ambaye alimwajiri kama mlinzi binafsi na baadaye kama mlinzi binafsi wa Carlos Pulecio Alcántara – kiongozi wa kwanza wa Kateli ya Kolonia Santita. Alcántara alipouwawa, Kahima alihamia kwa Panthera Tigrisi – Kiongozi Mkuu wa Kolonia Santita. "
152 " Hata wamisionari, hasa wamisionari wa Kiprotestanti, hawakukitumia Kiingereza katika kueneza dini kwa sababu hadhira yao isingewaelewa. Badala yake walitumia lugha za makabila ya Kiswahili, hivyo kujikuta wakieneza zaidi utamaduni wa Kiswahili kuliko wa Kiingereza au Kijerumani. "
153 " Meli ya kwanza kuondoka katika Bandari ya Salina Cruz kusini mwa Meksiko katika Bahari ya Pasifiki ni 'La Diosa de los Mares', 'Mungu wa Bahari', au 'Goddess of the Seas', Tani 6000, iliyoondoka saa tisa kamili usiku kuelekea Miami nchini Marekani; wakati ya mwisho kuondoka ilikuwa CSS ('Colonia Santita of the Seas', Tani 10000), na SPD ('El Silencio Depredador del Profundo', 'Mnyama Mtulivu wa Kina Kirefu', 'The Silent Predator of the Deep' – nyambizi ya Panthera Tigrisi), zilizoondoka saa kumi na moja alfajiri kuelekea Guatemala na Kolombia. Salina Cruz ni sehemu iliyopo kandokando mwa Bahari ya Pasifiki kusini kabisa mwa Meksiko na kaskazini-mashariki kwa Reparo Jicara katika jimbo la Oaxaca. Kambi ya Panthera Tigrisi ilijengwa ndani ya Msitu wa Benson Bennett – katika ufuko wa bahari kubwa kuliko zote ulimwenguni, iliyopuliza hewa na kuyumbisha miti anuai juu ya maabara kubwa kuliko zote katika Hemisifia ya Magharibi; ya kokeini, heroini, bangi, eksitasi na hielo ya China na Kolombia. Panthera Tigrisi alikamatwa katika Bahari ya Pasifiki. Kahima Kankiriho alikamatwa katika Msitu wa Bennett. "
154 " Mapema, kabla ndege haijaondoka na baada ya kuagana na maafisa waliomsindikiza, Nanda aliingia katika ndege na kutafuta namba ya kiti chake. Alivyoiona, alishtuka. Msichana mrembo alikaa kando ya kiti (cha Nanda) akiongea na simu, mara ya mwisho kabla ya kuondoka. Alivyofika, Nanda hakujizuia kuchangamka – alitupa tabasamu. Alivyoliona, kupitia miwani myeusi, binti alitabasamu pia, meno yake yakimchanganya kamishna. Alimsalimia Nanda, harakaharaka, na kurudi katika simu huku Nanda akikaa (vizuri) na kumsubiri. Alivyokata simu, alitoa miwani na kumwomba radhi Kamishna Nanda. Nanda akamwambia asijali, huku akitabasamu. Alikuwa na safari ya Bama kupitia Tailandi, kwa ndege ya Shirika la Ndege la Skandinavia na Maxair kutokea Bangkok; sawa kabisa na safari ya kamishna. "
155 " Wakati ndege inapaa huwa inapambana na upepo. Lakini inapaa, hata hivyo. "
156 " Kilometa mbili na ushei kidogo kutoka katika sanamu la Yesu Mtoto liitwalo Niñopa, katika Kanisa la Parokia ya Manispaa ya Xochimilco ('Sochimiliko') la Iglesia de San Bernardino de Siena, Mexico City, kulikuwa na nyumba ndogo ya siri ('safe house') ya Kolonia Santita iliyojengwa bila uzio wa ukuta au seng’enge isipokuwa miti iliyopandwa kuizunguka bila mpangilio wowote. Ndani ya nyumba hiyo Mpelelezi Maarufu Duniani John Murphy alikuwa akiteswa na magaidi kumi na mbili; waliokuwa wakiendelea kushangaa jinsi alivyookoka katika ajali ya ndege iliyoua watu zaidi ya mia tatu huko Uholanzi, na jinsi alivyoweza kuingia katika ofisi ya siri ya Panthera Tigrisi, kitu kilichomchanganya akili Tigrisi na makompade wote wa Kolonia Santita duniani kote. Bila Mtoto wa Rais wa Meksiko Debbie Patrocinio Abrego, na mwanasesere wa nyoka wa Mtoto wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Lisa Madrazo Graciano, John Murphy angeanguka. "
157 " Kuna mambo yanatokea hapa ulimwenguni ambayo yanafanya nikiri uwepo wa Mungu kwa asilimia kubwa. Wanasayansi wanasema ulimwengu ulianzishwa na mlipuko wa ‘Big Bang’, uliotokea takribani miaka bilioni 14 iliyopita, kutoka katika kitu kidogo zaidi kuliko ncha ya sindano, lakini hawatuambii nini kilisababisha mlipuko huo utokee au hicho kitu kidogo kuliko ncha ya sindano kilitoka au kilikuwa wapi. Wanaendelea kusema kuwa baada ya ‘Big Bang’ kutakuwepo na ‘Big Crunch’, ambapo ulimwengu utarudia hali yake ya awali ya udogo kuliko ncha ya sindano, na kila kitu kinachoonekana leo ulimwenguni hakitaonekana tena. Hapo sasa ndipo utata unapokuja. Mlipuko wa ‘Big Bang’ ulipotokea ulimwengu ulilipuka na kusambaa pande zote nne za ulimwengu kwa mwendokasi wa zaidi ya kilometa milioni 2 kwa saa, mpaka hivi leo unavyoonekana na bado unaendelea kusambaa. Kutokana na dhana ya ‘Big Crunch’, wanasayansi wanaamini ulimwengu utapanuka ila baadaye utapungua mwendo na utarudi mwanzo kabisa mahali ulipolipukia. Lakini mwaka 1995 wanasayansi hao hao waligundua kitu. Ulimwengu – badala ya kupungua mwendo wa kupanuka kama wanasayansi walivyokuwa wakitabiri – sasa unaongeza mwendo, tena kwa mwendokasi ambao haujawahi kutokea. Hiki ni nini kinachosababisha ulimwengu uongeze mwendokasi kiasi hicho badala ya kuupunguza? Hicho ni nini ambacho ulimwengu unapanukia? Wanasayansi hawana jibu. Wanasingizia kitu kinaitwa ‘dark matter’, maada ambayo haijawahi kuonekana, kwamba ndicho kinachosababisha ulimwengu uongeze mwendokasi kwa kiwango hicho ambacho hakijawahi kutokea; na hicho ambacho ulimwengu unapanukia wanahisi ulimwengu wetu unapanukia katika ulimwengu mwingine, kwa mujibu wa dhana nyingine kabisa iitwayo ‘multiverse’ au ‘meta-universe’. Kuna kitu kinaitwa ‘Higgs boson’ – chembe ndogo inayosemekana kuhusika na uzito (‘mass’) wa chembe ndogo 16 zilizomo ndani ya atomu, kasoro chembe ya mwanga, iliyopotea mara tu baada ya mlipuko wa ulimwengu wa ‘Big Bang’ miaka bilioni 13.7 iliyopita katika kipindi kilichoitwa ‘epoch’ – ambayo ilianza kutafutwa katika maabara za CERN, Uswisi, toka mwaka 1964, maabara ambazo kazi yake kubwa ni kutengeneza mazingira ya mwanzo kabisa ya mlipuko wa ‘Big Bang’, kusudi wanasayansi waone kama wanaweza kubahatisha kuiona na kuidhibiti hiyo bosoni. Bosoni itakapopatikana wanasayansi watajua siri ya ‘dark matter’, watajua jinsi ulimwengu unavyofanya kazi na jinsi ulivyoumbwa na jibu la kitendawili cha ‘Standard Model’ litapatikana. Hiyo ni kazi ngumu. Ndiyo maana ‘Higgs boson’ mwaka 1993 iliitwa ‘The God Particle’. Yaani, wanasayansi wanahisi kuna muujiza wa Kimungu na huenda wasiipate kabisa hiyo bosoni. Wanasema waliipata mwaka 2013. Lakini hiyo waliyoipata bado ina utata. Kutokana na kushindwa huko kwa sayansi na historia, kutokana na kushindwa kwa sayansi kutengeneza binadamu au mnyama, kutokana na miujiza iliyorekodiwa katika vitabu vitakatifu; naamini, Mungu yupo. "
158 " Wanasayansi wana uwezo wa kupeleleza hadi kipindi cha karne ya kwanza ambapo Yesu aliishi, alikufa, alifufuka na alipaa kwenda mbinguni, na wana uwezo wa kujua mambo mengi kwa hakika yaliyofanyika katika kipindi hicho na hata katika kipindi cha kabla ya hapo. Kuna miujiza ambayo Yesu aliifanya ambayo haiko ndani ya Biblia. Kwa mfano, Biblia inasema Yesu alizaliwa ndani ya zizi la ng’ombe wakati sayansi inasema alizaliwa nje ya zizi la ng’ombe; na muujiza wa kwanza kuufanya ambao hauko ndani ya Biblia ni kutembea mara tu baada ya kuzaliwa, na watu na ndege wa angani kuganda kabla ya kuzaliwa Masihi na kabla ya wakunga kufika kumsaidia Maria Magdalena kujifungua. Akiwa na umri wa miaka sita, sayansi inasema, Yesu alikuwa akicheza na mtoto mwenzake juu ya paa la nyumba ya jirani na mara Yesu akamsukuma mwenzake kutoka juu hadi chini na mwenzake huyo akafariki papo hapo. Watu walipomsonga sana Yesu kwa kumtuhumu kuwa yeye ndiye aliyesababisha kifo cha mwenzake, na kwamba wangemfungulia mashtaka, Yesu alikataa katakata kuhusika na kifo hicho. Lakini walipozidi kumsonga, aliusogelea mwili wa rafiki yake kisha akamwita na kumwambia asimame. Yule mtoto alisimama! Huo ukawa muujiza mkubwa wa kwanza wa Yesu Kristo, kufufua mtu nje ya maandiko matakatifu. Kuna mifano mingi inayodhihirisha uwepo wa Mungu ambayo wanasayansi hawawezi hata kuipatia majibu. Tukio la Yoshua kusimamisha jua limewashangaza wanasayansi hadi nyakati za leo. Mwanzoni mwa miaka ya 70 wanasayansi walijaribu kurudisha muda nyuma kwa kompyuta kuona kama kweli wangekuta takribani siku moja imepotea kama ilivyorekodiwa katika Biblia. Cha kushangaza, cha kushangaza mno, walikuta saa 23 na dakika 20 zimepotea katika mazingira ambayo hawakuweza na hawataweza kuyaelewa. Walipochunguza vizuri walikuta ni kipindi cha miaka ya 1500 KK (Jumanne tarehe 22 Julai) ambacho ndicho tukio la Yoshua la kusimamisha jua na kusogeza mwezi nyuma digrii 10, ambazo ni sawa na mzunguko wa dakika 40, lilipotokea. Kwa kutumia elimu ya wendo, elimu ya kupanga miaka na matukio ya Kibiblia, dunia iliumbwa Jumapili tarehe 22 Septemba mwaka 4000 KK. Hata hivyo, mahesabu ya kalenda yanaonyesha kuwa Septemba 22 ilikuwa Jumatatu (si Jumapili) na kwamba kosa hilo labda lilisababishwa na siku ya Yoshua iliyopotea. Hayo yote ni kwa mujibu wa Profesa C. A. Totten, wa Chuo Kikuu cha Yale, katika kitabu chake cha ‘Joshua’s Long Day and the Dial of Ahaz: A Scientific Vindication and a Midnight Cry’ kilichochapishwa mwaka 1890. Kama hakuna Mungu iliwezekanaje Yoshua aombe jua lisimame na jua likasimama kweli? Iliwezekanaje Yesu aseme atakufa, atafufuka na atapaa kwenda mbinguni na kweli ikatokea kama alivyosema? Ndani ya Biblia kuna tabiri 333 zilizotabiri maisha yote ya Yesu Kristo hapa duniani na zote zilitimia – bila kupungua hata moja. Utasemaje hapo hakuna Mungu? Mungu yupo, naamini, sijui. Tukio la Yesu kufa, kufufuka na kupaa kwenda mbinguni si la vitabu vitakatifu pekee, hata sayansi inakubaliana na hilo. "
159 " WWPP ('WODEA Witness Protection Programme') ni Programu Maalumu ya Ushahidi ya Tume ya Dunia ya kuwakinga mashahidi wa kihalifu kwa kuwapa makazi mapya, majina mapya, kazi mpya, historia mpya ya maisha, na sura mpya, kuwakinga na Sheria ya Kitalifa ya Kolonia Santita. Ukivunja Sheria ya Kitalifa ya Kiapo cha Swastika cha Kolonia Santita utauwawa, tena utauwawa kinyama, wewe na familia yako. "
160 " Hatutakiwi kuishi kama raia wa Tanzania peke yake. Tunatakiwa kuishi kama raia wa dunia na watumishi wa utu, hasa katika kipindi hiki cha zama za utandawazi. Sina lazima ya kutoka nje kufanya utafiti wa kazi zangu siku hizi. Nje ninayo hapa ndani! "