Home > Author > Enock Maregesi
61 " Nini kingetokea kama Adamu na Hawa wasingekula tunda la Mti wa Maarifa ya Mema na Mabaya mpaka siku ya Sabato? Mungu angewaruhusu kula na lengo la uumbaji wa Mungu lingekamilika. Wanadamu wakifuata Amri Kumi za Mungu katika maisha yao watakuwa na uwezo maalumu ambao baadaye utawawezesha, kupitia Roho Mtakatifu, kuwa na maarifa ya siri ya uumbaji wa Mungu. "
― Enock Maregesi
62 " Ndoto za wachawi ni tofauti kidogo na ndoto takatifu. Wachawi wanapokuwa hawahitaji kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine, lakini wana hamu ya kuona wenzao wanafanya nini au wanasema nini, huwa wanalala ubavu mmoja upande wa kushoto kwa jina la mungu wao na la mashetani wote. Kisha wanatoa mvuke wa bluu midomoni mwao. Kupitia mvuke huo, kwa nguvu za Shetani na kwa ruhusa ya Mwenyezi Mungu, wataona na watasikia kila kinachofanyika upande wa pili. Kile wanachotaka kukiona na kukisikia hujifunua katika ufahamu wao kama taswira au maono, kutoka katika akili isiyotambua, ya watu wakifanya au wakisema kitu. Kama wanataka kujua siri za watu wengine, hata wale ambao si wachawi, watazijua kupitia ndoto hizo; kwa sababu ya makubaliano ya wazi, si ya siri, waliyoingia na Shetani. Makubaliano hayo si ya lelemama; yaani yale ambayo hufanywa kwa kutoa kafara ya mnyama, au kufuru ya aina yoyote ile kwa Mwenyezi Mungu, au kwa kuabudu dini za kichawi. Lakini ni kwa sadaka halisi ya wao wenyewe ya mwili na roho kwa Shetani na kwa kufuru ya kuikana kabisa, imani ya Mwenyezi Mungu. Lakini hiyo ni kwa wale wanaotumia uchawi wa kishetani. Wale wanaotumia uchawi wa asili, kama vile kutumia risasi kumroga mtu kwa sababu risasi mungu wake ni sayari ya Zohali, au wale walioingia mkataba wa siri na Shetani, hawana uwezo wa kuota hivyo. Hivyo, si kila mchawi anaweza kuota ndoto za namna hiyo, ni kwa wale tu walioingia mkataba wa wazi na Shetani. "
63 " Mammon ni mungu wa pesa wa kuzimu anayesimamia mambo yote ya kifedha ulimwenguni. Ni miongoni mwa mashetani saba waliotupwa na Mwenyezi Mungu hapa duniani kutokea mbinguni akiwemo Ibilisi, Beelzebub, Asmodeus, Leviathan, Amon na Belphegor. Ibilisi ni mungu wa kiburi, Beelzebub ni mungu wa uroho, Asmodeus ni mungu wa zinaa, Leviathan ni mungu wa wivu, Amon ni mungu wa hasira na Belphegor ni mungu wa uvivu. Jukumu la mashetani hawa ni kusimamia kwa uaminifu mkubwa kutokea kuzimu dhambi kubwa saba duniani ambazo ni kiburi, uroho, zinaa, wivu, hasira, uvivu na uchoyo. Dawa ya dhambi hizo ni busara, kiasi, ujasiri, imani, haki, tumaini na upendo. "
64 " Tunazaliwa, kuteseka na kufa kwa sababu ya dhambi ya asili ya wazazi wetu wa kwanza (Adamu na Hawa). Kama Hawa asingekubali kudanganywa na Shetani, tungezaliwa bila uchungu, tungeishi bila kuteseka na tusingekufa milele. Lakini haya ndiyo mawazo yangu: Mungu Ahusiki na dhambi, Ahusiki na mwili, Anahusika na roho. Hivyo, mtu anapofariki mwili unabaki duniani lakini roho inarudi kwa Mungu; kwani Yeye ndiye aliyeitengeneza na kuiweka katika moyo wa mtu. Mimi na wewe ni viumbe vyenye thamani kubwa sana mbele za Mwenyezi Mungu; mapenzi Yake kwetu hayana masharti yoyote. Hainiingii akilini (hata kidogo) kumtesa mtu unayempenda kiasi hicho milele, wakati uwezo wa kumwokoa unao. "
65 " Dhambi ya Adamu ilileta mauti duniani (kwa viumbe vyote, si tu kwa binadamu). Hiyo ni kwa mujibu wa Biblia. Kisayansi si kweli; kwa sababu mauti yalikuwepo kabla Adamu na Hawa hawajaumbwa! Lakini haya ndiyo mawazo yangu: Dhambi iliathiri uumbaji wote ikiwemo mimea, wanyama, wadudu na kila kitu kilichoumbwa na Mwenyezi Mungu; ambavyo huteseka kwa sababu ya laana ya dunia. Kama wanyama na mimea visingekuwa vinakufa, binadamu wasingepata mahali pa kuishi. Hata hivyo, kifo cha Yesu msalabani kitafufua kila kitu – kitafufua uumbaji wote. "
66 " Matatizo ya kijamii, kimiiko, kimaadili, kisiasa, na kiroho; hayataweza kutatuliwa kwa pesa, vikao vya kifamilia, haki za binadamu, usalama wa taifa, au nguvu za kijeshi. Yataweza kutatuliwa kwa haki na hekima ya Mwenyezi Mungu. "
67 " Mtu akikuita mjinga au mpumbavu juu ya maisha yako usikasirike kwa sababu wewe si mjinga wala mpumbavu. Sema hapana kwa ndiyo nyingi kwa sababu hawapaswi kuingilia mambo ya mtu mwingine bila idhini ya Mwenyezi Mungu. Kuingilia mambo ya mtu mwingine bila idhini ya Mwenyezi Mungu ni dhambi, tena dhambi kubwa, ni kuvunja amri kuu ya kwanza ya Mungu. "
68 " Maendeleo ya mtu yatatokana na juhudi za mtu mwenyewe. "
69 " Tumaini lina nguvu kuliko woga… Usisimame. Endelea kutembea. "
70 " Musa alipokuwa mlimani kupokea Amri Kumi za Mungu kwa ajili ya Wana wa Israeli alikawia sana kurudi, kiasi cha watu kukata tamaa na kujiona wapweke wakiwa njiani kuelekea katika Nchi ya Ahadi. Kutokana na woga usio na kifani na kukata huko kwa tamaa waliamua kutosubiri tena kusikia neno kutoka kwa Mungu, au kuiona sura halisi ya Mungu kama Musa alivyokuwa amewaahidi, hivyo wakamlazimisha Haruni awatengenezee mungu kutokana na taswira ambayo tayari walishakuwa nayo vichwani mwao kuhusu mungu waliyemtaka; yaani ndama wa dhahabu, au mungu mpya ambaye angewapa chochote walichotaka muda wowote waliotaka. "
71 " Usiwapoteze marafiki zako wa mwanzo kwa sababu ya ujinga wako, wala usiwaache marafiki zako wa mwanzo kwa sababu ya ujinga wao. "
72 " Marafiki zako wa mwanzo ni wazuri kuliko wote. "
73 " Marafiki zako wa mwanzo ambao bado ni marafiki zako mpaka sasa ni wazuri kuliko wote kutokana na sababu mbalimbali: Wamekuwepo pamoja nawe katika shida na raha; wanakujua vizuri unapokuwa na furaha, na wanakujua vizuri unapokuwa na huzuni; mmezoeana kwa miaka mingi na wanaujua hata utani wako wa ndani; wanajua nini unapendelea zaidi na nini hupendelei zaidi, na wanazijua sifa zako za ushupavu na sifa zako za udhaifu. Hata hivyo, katika maisha yetu, tunahitaji marafiki wa aina zote mbili kurahisisha maisha. Marafiki wapya hutuongezea viungo muhimu katika maisha yetu wakati marafiki wa mwanzo ni nguzo au miamba imara ya maisha yetu, na ndiyo watu hasa watakaotusaidia katika shida na raha! Usiwapoteze au usiwaache marafiki zako wa mwanzo lakini jenga mahusiano mapya. Marafiki zako wa mwanzo ni dhahabu, wa sasa ni fedha. "
74 " Ghillie ni mavazi yaliyotumiwa na makomandoo wa Tume ya Dunia ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya (Frederik Mogens, Radia Hosni, Daniel Yehuda na John Murphy) kama mbinu ya kujificha kwa kujifananisha na rangi au maumbo ya mazingira ya Msitu wa Benson Bennett, kama afanyavyo kinyonga. Hata hivyo, walivyoingia katika jumba la utawala katika maabara za Kolonia Santita ndani ya Msitu wa Benson Bennett katika mji wa Salina Cruz, Vijana wa Tume walivua suti zao za ghillie; kusudi iwe rahisi kwao kupambana na jeshi binafsi la Kolonia Santita, liitwalo 'autodefensa'. "
75 " Potassium Cyanide si hatari inapokuwa nje. Ni hatari inapojichanganya na asidi za tumboni ambapo hubadilika na kuwa gesi ya 'hydrogen cyanide'. Gesi ya 'hydrogen cyanide' ni miongoni mwa sumu hatari zaidi ulimwenguni. Mtu akimeza kidonge cha 'cyanide' atapata madhara makubwa. Kichwa chake kitamuuma hapohapo na atachanganyikiwa akili. Ngozi yake itakuwa nyekundu, kwa sababu damu yake itakuwa nyekundu zaidi – kutokana na kuzidi kwa oksijeni katika damu. Mwili hautakuwa na uwezo tena wa kuchukua oksijeni kutoka katika damu ili uitumie, kwa hiyo damu itazidi kuwa na oksijeni zaidi. Atapumua kwa shida. Mapafu yake yatafanya kazi vizuri lakini mwili wake hautakuwa na uwezo wa kutumia oksijeni yoyote – hivyo atadhani ana matatizo katika mfumo wake wa kupumua. Atazimia. Yaani, oksijeni haitafika kwenye ubongo. Atapata kifafa na atatapika nyongo. Ubongo wake utashindwa kufanya kazi na atakuwa mahututi ndani ya sekunde kumi! Baada ya hapo moyo wake utasimama kufanya kazi, na atafariki dunia. "
76 " Mapenzi, kama ilivyo kwa vitu vyote hapa ulimwenguni, hayawezi kuwepo bila kujumuishwa na fizikia na kemia yake! Bila kemia hakuna mapenzi ya kudumu. Tamaa ya ngono kimsingi huanza pindi unapokutana na mtu. Tamaa hiyo huweza kukua na kuwa kitu kingine kadiri muda unavyokwenda lakini chanzo kinakuwepo toka siku ya kwanza mlipokutana. Kemikali inayosababisha tamaa ya ngono na hata kuikuza tamaa hiyo ni 'phenyl ethylamine' ('fino itholamine') au PEA ambayo ni kemikali ya mapenzi ndani ya ubongo. Husisimua watu na huongeza nguvu za kimwili (fizikia) na kihisia (kemia). Tamaa husababisha mtu azalishe PEA nyingi zaidi, kitu kinachosababisha kujisikia kizunguzungu (cha hisia za kimapenzi) na dalili zingine kama magoti kutetemeka, jasho kutoka viganjani na kutokutulia. Kemikali hii inapozalishwa kwa kiwango kikubwa, hutuma alamu ('signals') kutoka kwenye ubongo mpaka kwenye viungo vingine vya mwili na kutumika kama 'dopamine' au 'amphetamine' ambazo ni kemikali za ulevi ndani ya ubongo. Iwapo unajiuliza kwa nini wewe au mtu mwingine unavutiwa na mtu ambaye hamwendani kimapenzi, inaweza kuwa ni kwa sababu una kiwango kikubwa cha kemikali hizo kuliko mwenzako, kitu ambacho huzidi uwezo wa kutumia kichwa na kutoa maamuzi bora kulingana na akili ya kuzaliwa.Kwa jumla, mapenzi yote ya kweli uhitaji angalau kiwango kidogo cha PEA kwa wale wanaopendana. Cha msingi kukumbuka ni kwamba kemikali hizi huja kwa vituo, nikiwa simaanishi kwamba tamaa ya ngono hupotea pale mtu anapoelekea kwenye uhusiano wa kudumu. Lakini mambo hubadilika. Hatuwezi kuvumilia zile hisia kali kadiri tunavyozidi kusafiri kuelekea kwenye uhusiano wa kudumu na kwenye maisha ya pamoja yenye furaha. Katika uhusiano wenye afya hata hivyo matatizo hutokea hapa na pale. Chanzo cha Murphy na Debbie kupendana kilikuwa kemia zaidi kuliko fizikia. Kama hakuna kemia hakuna mapenzi. "
77 " Luka 22:20 ni mwisho wa agano la kale la damu za wanyama na mwanzo wa agano jipya la damu ya Yesu. "
78 " Hakuna mahali popote katika Agano Jipya ambapo sheria ya Sabato imekomeshwa (Kutoka 31:12-17), kwani Mungu alianzisha Sabato kwa ajili ya wanadamu wote (Marko 2:27). Kinyume cha hapo, Yesu aliitunza (Luka 4:16), Paulo aliitunza (Matendo 17:2) na Wamataifa waliitunza pia (Matendo 13:42-44; 16:13)! Mwandishi wa Waebrania anaandika bila kificho, “Basi, imesalia raha ya Sabato kwa watu wa Mungu” (Waebrania 4:9). "
79 " Gari ya Debbie huchukua sekunde 12 kutoka kilometa 0 mpaka kilometa 210 kwa saa. Huchukua sekunde 10 kutoka kilometa 210 kwa saa mpaka kilometa 0. Ina uwezo wa kusimama haraka kuliko inavyoweza kukimbia. "
80 " Mpelelezi wa Tume ya Dunia kutoka Israeli Daniel Yehuda Ben-Asher Ebenezer, Mhebrania aliyeishi Givat Ram, Jerusalem, na mke wake mrembo Hadara na mtoto wake mzuri Navah Ebenezer, alikuwa Ukanda wa Gaza siku alipopigiwa simu na Kiongozi wa Kanda ya Asia-Australia ya Tume ya Dunia U Nanda – kutoka Copenhagen kuhusiana na wito wa haraka wa kuonana na Rais wa Tume ya Dunia. Yehuda aliondoka usiku kwenda Yangon, Myama, ambapo alionana na U Nanda na kupewa maelekezo yote ya kikazi aliyotakiwa kuyafuata. Mbali na maelekezo yote ya kikazi aliyotakiwa kuyafuata, Nanda alimkabidhi Yehuda kachero wa Kolonia Santita Mandi Dickson Santana (bila kujua kama Mandi ni kachero wa Kolonia Santita) ili amsindikize mpaka stendi ya mabasi ya Maubin, nje ya Yangon. Baada ya hapo Yehuda alisafiri mpaka Copenhagen ambapo yeye na wenzake walikabidhiwa Operation Devil Cross, ya kung’oa mizizi ya Kolonia Santita duniani kote. Yehuda alifanya kosa kubwa kuonana na kachero wa Kolonia Santita Mandi Santana! Kwa sababu hiyo, sauti na picha ya Yehuda vilichukuliwa, watu wengi walikufa katika miji ya Copenhagen na Mexico City. "